Tuesday, August 30, 2016

Dikteta

::Madikteta wote duniani hufanana::

Kutoka Maktaba (JF by Mzee Mwanakijiji 
11 Feb 2011 ) #UKUTA

Madikteta wote wanafanana; wawe ni wale ambao ni mtu mmoja mmoja au wawe wa chama kimoja; kufanana kwao kunatabiri vitendo vyao. Hufanana katika mambo makubwa matano:

a. Huamini kuwa wao ndio pekee wenye uwezo wa kutawala (Katika fikra zao hawaamini kama kuna mtu au chama kingine kinachoweza kutawala vizuri kuliko wao). Baadhi yao (kama ni mtu mmoja au chama) hujiaminisha kabisa kuwa ni wateule wa Mungu kutawala nchi zao.
b. Huamini kuwa wanapendwa sana kupita kiasi (hili kuelezea kwanini picha, sanamu, n.k zao huenezwa kila kona ya nchi) Hupenda kuimbiwa nyimbo za kusifiwa na kupeperushiwa maua kila wapitapo kama ishara ya "upendo" huu.
c. Hawako tayari kuamini wanaweza kukataliwa; Mara zote inapotokea mtu anawapinga au kuwakataa hutafutiwa sababu ya kuoneshwa kuwa haiwezekani awakate wao kwani (b) wao wanapendwa sana!
d. Hata siku moja hawajawahi kutengeneza mifumo itakayowaondoa wao wenyewe madarakani. Hivyo, hutumia mbinu zote kufanya mabadiliko ya kimapambo tu ambayo kwa watu wasiofuatilia huweza kuvutiwa kuwa ni mabadiliko. HIvyo aidha hujikuta wanaondoka kwa kukimbia au kwa kukimbizwa na wananchi wao au mataifa ya nje!
e. Wako tayari kufanya jambo lolote kubakia madarakani - msisitizo hapa uko kwenye neno "LOLOTE".

Kutokana na hayo matatu tabia za madikteta wote huweza kutabirika (wawe ni mtu mmoja au chama kimoja). Na ili kuhakikisha hayo matatu madikteta wote duniani (wanaovaa nguo za kiraia na wale wanaovaa nguo za kijeshi)

1. Hutumia vitisho kulazimisha kupendwa na kukubalika - silaha ya dikteta ni vitisho (terror). Wakikukamata watakasumbua sana hadi uogope. Lengo ni kukushawishi uone ni kwanini wao wanastahli kupendwa! Hupenda kujiona kama wazazi wa wananchi - nani atamchukia mzazi wake?
2. Hutengeneza masimulizi ya sifa na kuyalazimisha yaaminiwe hata kama msingi wake ni uongo. Madikteta ni mabingwa wa kuunda (manufacture) uongo. Uwezo wao mkubwa wa kufanya hivi hutokana na ukweli kuwa wao humiliki vyombo vya habari vyenye kufikia watu wengi zaidi (radio, TVs n.k)
3. Inapofikia mahali kuwa upendo wa wananchi unapungua au wanaanza kuwa na mashaka nao madikteta huanza kupoteza watu. Yaani, pole pole watu huanza kukamatwa na kuwekwa "vizuizini" ili wasimpinge sana dikteta.
4. Kisingizio pekee cha madikteta wote (wawe wa mtu mmoja au chama kimoja) kuhalalisha kuwanyanyasa, kuwanyima wananchi uhuru na hata kuwatia watu nguvuni ni "kwa ajili ya nchi". Yaani, hutumia "taifa" kama kisingizio cha wao kuendelea kutawala.

Kwanini?

Kwa sababu madikteta wote wanataka kupendwa na kukubaliwa!

Ole wao wananchi wanaposema "hapana"!

Share this

0 Comment to "Dikteta"

Post a Comment