Miaka 10 ya ndoa yetu siku moja niliingia
nyumbani nikamkuta mke wangu akiniandalia chakula cha usiku. Nilimshika mkono na kumwambia: “Nina jambo ninalotaka kukueleza.” Alikaa na kunisikiliza kwa makini. Dalili za wasiwasi nilikuwa nikizishuhudia machoni mwake. Ghafla nilijikuta katika hali ya kushindwa kukifungua kinywa changu. Lakini ilikuwa ni lazima ajue ninachokifikiria, hivyo nilipiga moyo konde, nikamwambia kwa upole: “Ninataka tuachane.” Hakuonekana kuudhika kwa hoja niliyokuwa nimeiwasilisha mbele yake, bali aliniuliza kwa sauti ya upole kabisa: “Kwa nini?” Nilijaribu kulikwepa hilo swali, hivyo alighadhibika sana na kuniambia kwa sauti ya juu: “Wewe si mwanaume!” Usiku ule hatukusemeshana, na muda wote alikuwa akilia. Nilitambua kuwa alitaka kujua kitu gani kimetokea katika ndoa yetu. Lakini sikuweza kumpa jibu lenye kuridhisha; kwa sababu sikuwa na mapenzi naye tena, moyo wangu ulikuwa umetekwa na binti mwingine aitwaye Jane. Nilimsikitikia sana! Huku nikiwa na hisia za hatia moyoni mwangu, niliandika pendekezo la talaka ambalo lilieleza kuwa atachukua nyumba yetu, gari na shea ya asilimia 30 ya kampuni yangu. Mke wangu aliitazama karatasi hiyo kisha akaichana na kuitupa kwenye ndoo ya takataka. Huyu ni mwanamke aliyekuwa ameishi nami kwa muda wa miaka kumi alikuwa amegeuka kuwa kama mgeni kwangu. Nilisikitika sana na kumuomba radhi kwa kumpotezea muda, rasilimali na nguvu zake lakini sikuweza kutengua kauli yangu kwa sababu nilikuwa nikimpenda sana Jane na nilikuwa nimezama kweli kweli ndani ya huba lake na kuwa teja wa penzi lake. Hatimaye alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo nilikuwa nikitarajia kuliona. Kilio chake kwangu kilikuwa kama faraja. Wazo la talaka lililonitawala kwa wiki kadhaa lilikuwa likizidi kupata nguvu na sasa lilionekana kuwa wazi kabisa. Siku iliyofuata nilirudi nyumbani nikiwa nimechelewa na kumkuta akiandika kiandika kitu mezani. Sikutaka kula chochote zaidi ya kuelekea moja kwa moja kitandani kwa sababu nilikuwa nimechoka sana kutokana na mishemishe za siku hiyo nikiwa na Jane. Niliposhtuka, bado alikuwa hajatoka mezani. Sikujali hata kidogo, nikageuka na kuendelea kuuchapa usingizi. Asubuhi alinipatia masharti ya talaka: hakutaka mali yoyote kutoka kwangu, bali alitaka kuwe na muhula wa mwezi mmoja kabla ya talaka. Alitaka kwamba katika kipindi hicho tujaribu kuishi kama kawaida kwa kadiri iwezekanavyo. Hoja yake ilikuwa wazi: mtoto wetu alitarajia kufanya mitihani ya shule ndani ya mwezi huo na hakutaka tumchanganye kwa tukio la talaka. Hili nililikubali. Lakini alikuwa na nyongeza : alinitaka nikumbuke siku ya ndoa yetu nilipomnyanyua kumpeleka chumbani kwetu. Alitaka kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mzima niwe nambeba kila siku asubuhi kumtoa chumbani mpaka mbele ya mlango wa nje ya nyumba. Nilihisi kuwa alikuwa ameshikwa na wendawazimu. Nilikubali ombi lake kwa sababu niliona kuwa mwezi mmoja sio kitu, kwani nilitaka tuachane. Nilimsimulia Jane kuhusu masharti ya talaka yaliyotolewa na mke wangu. Alicheka sana na kuona kuwa ni upuuzi. “Hata akitumia hila gani lazima apewe talaka,” alisema Jane kwa masihara. Tangu nilipoelezea nia yangu ya kutaka kuachana naye, hatukuwa na uhusiano wa kimwili na mke wangu. Hivyo nilipombeba siku ya kwanza, sote tulionekana kutokuwa na uchangamfu. Mtoto wetu alifurahi na kupiga makofi: “Baba amembeba mama”. Kauli yake ilinipa maumivu moyoni. Kutoka chumbani mpaka barazani, kisha mlangoni, nilitembea mita kumi nikiwa nimembeba mikononi mwangu. Aliyafumba macho yake na kuniambia kwa upole na ulaini: “Usimwambie mtoto wetu kama tunaachana.” Nilikubali kwa kutikisha kichwa huku nikiwa nimefadhaika. Nilipofika nje nilimshusha akaenda kituoni kusubiri basi, nami nikachukua gari langu na kwenda ofisini nikiwa peke yangu. Siku ya pili tulijaribu kutoonesha hali yoyote ya mifarakano. Aliegemea kifuani kwangu nikahisi manukato mazuri ya blauzi yake. Nilibaini kuwa sikuwa nimemtazama vizuri mke wangu kwa muda mrefu. Uso wake ulikuwa umeanza kuwa na mikunjo na nywele zake zilikuwa zimeanza kubadilika. Ndoa yetu ilikuwa imemfanya achoke. Kwa dakika kadhaa niliduwaa na kuwaza kile nilichokuwa nimemfanyia. Siku ya nne nilipombeba nilihisi aina ya ukaribu na mvuto ikirejea. Huyu ni mwanamke aliyekuwa amenipa miaka kumi ya uhai na maisha yake. Siku ya tano na ya sita, kwa mara nyingine, niliona hali ya ukaribu na mvuto fulani ikirejea kati yetu. Sikumsimulia Jane kuhusu hali hii. Kadiri siku zilivyosonga mbele ndivyo nilivyozidi wepesi wa kumbeba. Yumkini ilisababishwa na ile hali ya kumbeba kila siku kiasi cha kumuona kuwa ni mwepesi. Asubuhi moja alikuwa akichagua nguo ya kuvaa. Alijaribu nguo kadhaa lakini hakupata inayomfaa . Alishusha pumzi na kusema: “Nguo zangu zote hazinienei, zimekuwa kubwa”. Nilibaini kuwa alikuwa amekonda na ndiyo maana niliweza kumbeba kwa urahisi. Nilisikitika kwa sababu nilihisi kuwa alikuwa amebeba mambo mengi moyoni mwake. Hivyo nilimsogelea na kukipapasa kichwa chake. Ni wakati huo ambapo mtoto wetu aliingia na kusema: “Baba sasa ni muda wa kumbeba mama”. Tukio la kumuona baba yake akiwa amembeba mama yake lilimuathiri na kuwa sehemu muhimu sana ya maisha yake. Mke wangu alimuita na kumkumbatia kwa upendo. Niligeuza uso wangu pembeni, sikutaka kuangalia tukio hilo nisinje nikabadilisha uamuzi wangu wa talaka. Nilimnyanyua na kumbeba mke wangu, nikatembea kutoka chumbani, sebuleni mpaka nje. Aliizungusha mikono yake mizuri shingoni kwangu, nami nikamshikilia vizuri; ilikuwa kana kwamba ni siku ile ya harusi yetu. Lakini wepesi wa mwili wake ulinifanya niwe mwenye huzuni. Siku ya mwisho nilipombeba niliingiwa na uzito wa kupiga hatua. Wakati huo mtoto wetu tayari alikuwa shule. Nilimshikilia vizuri na kusema: “Sikuwa nimejua kuwa maisha yetu yamekosa mvuto”. Niliwasha gari kuelekea ofisini, niliamua kupita kwa Jane. Nilipofika nilitoka bila hata kuubana mlango wa gari. Nilikuwa na wasiwasi nisije nikaghairi nia yangu… nikapandisha ngazi. Jane alipofungua mlango nilimwambia: “Samahani Jane, sitaki kuachana na mke wangu”. Alinitazama kwa mshtuko na kunigusa kwenye paji la uso. “Una homa?” alisema. Niliutoa mkono wake na kumwambia: “Samahani Jane, sitaki kumuacha mke wangu. Yawezekana maisha yangu na mke wangu yalikosa uchangamfu kwa sababu hatukuwa karibu, sio kwa sababu hatukupendana. Sasa nimebaini kwamba kwa kuwa nilimbeba siku ya ndoa yetu, ninapaswa kuendelea kufanya hivyo mpaka kifo kitutengenishe.” Jane alionekana kushtuka sana. Alinizaba kibao, akaubamiza mlango na kuanza kulia. Nilimuacha nikapanda gari na kuondoka. Njiani nilipita kwenye duka la maua nikaagiza shada la maua kwa ajili ya mke wangu. Muuzaji akaniuliza ujumbe unaotakiwa kuandikwa juu ya kadi nikatabasamu na kumwambia aandike: “Kila siku asubuhi nitakubeba mpaka kifo kitakapotutenganisha”. Jioni nilifika nyumbani nikiwa na maua mkononi, tabasamu usoni, nikapandisha ngazi mpaka ndani. Nilipofika chumbani mke wangu alikuwa amelala akiwa amefariki dunia. Kumbe alikuwa akipambana na KANSA kwa miezi kadhaa lakini sikujua kwa sababu nilikuwa nimetekwa na Jane. Bila mimi kufahamu, kumbe marehemu mke wangu alijua kwamba muda si mrefu atafariki dunia na alitaka kuniokoa dhidi ya fikra yoyote mbaya kutoka kwa mtoto wetu kama tungeachana muda mfpi kabla ya kifo chake. Angalau machoni mwa mwanangu naonekana kuwa mume mwenye upendo… WAPENDANAO NATAKA MJIFUNZE 1) Wengi wanatengana si kwa sababu hawapendani, bali hawapeani muda wa kusikilizana. 2)Wengi wanaamini ukiachana na mpendwa wako ni lazima muwe maadui. 3)Busara ndani ya pendo ni zaidi ya mali na pesa. |
0 Comment to "My Dream Safari 2060"
Post a Comment